03 December 2013

MAGUFULI: SINA HURUMA KWA MATAJIRI WA MAGARI



Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, amesema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973 hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara, anaripoti Goodluck Hongo.

Dkt. Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hafla ya kutilia saini mikataba mitatu ya ujenzi wa barabara za Dodoma- Manyara inayopita Mayamaya- Babati-Bonga.
Barabara nyingine ni Tunduru- M a n g a k a - Mtambaswala na kusema kuwa, barabara hizo z i n a j e n gwa kwa gharama kubwa hivyo watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi kupitia
 Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), wanapaswa kusimamia sheria.
Alisema usimamizi makini wa sheria za barabara, utasaidia kuzifanya zidumu zaidi kwani Rais Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara hiyo kusimamia sheria ambapo kitendo cha wamiliki wa magari kuzidisha uzito, kinamchukiza sana.
“Sipo tayari kuona matajiri wachache wakiharibu barabara na kujipatia faida kubwa wakati barabara hizi zinajengwa kwa mkopo unaolipwa na kodi za wananchi.
“Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, mimi nitaendelea kusimamia sheria hadi naingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari yanayozidisha uzito na kuharibu barabara,” alisema Dkt. Magufuli.
Aliongeza kuwa, kama matajiri hao wataachiwa waendelee kuzidisha uzito, barabara zilizopo hazitadumu kwa muda mrefu na wananchi maskini wataendelea kulipa kodi.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema.
Akiwazungumzia wakandarasi waliochukua zabuni ya ujenzi wa barabara hizo, Dkt. Magufuli aliwaonya na kusisitiza kama hawawezi kazi ni bora wasisaini mikataba hiyo ili watafute wakandarasi wengine wenye uwezo.
Alisema kama wamekubali kusaini, wanapaswa kuanza kazi mara moja kwani Serikali ndio iliyokopa na walipakodi ni Watanzania hivyo si kukaa miezi sita ndio waanze kazi.
“Mameneja wa TANROADS katika mikoa ambayo miradi hii inafanyika, lazima msimamie kikamilifu ujenzi huu na kama mradi ukisuasua katika eneo lako ujue hutufai kufanya kazi hivyo uondoke mara moja,” alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, Bw. Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi na kuwajengea barabara na daraja la Mto Malagarasi ambapo yeye si mhafidhina; bali kama serikali imefanya mema inapaswa kupongezwa.
“Jema ni jema tu hata kama likifanywa na nani hivyo mimi si mhafidhina, kama Serikali imefanya mema basi inapaswa kupongezwa,” alisema.
Aliongeza kuwa, licha ya Serikali kuwajengea Daraja la Mto Malagarasi, bado barabara zingine ikiwemo ya Nyakanazi ina hali mbaya, hivyo pamoja na kuipongeza serikali kwa kusaini mikataba hiyo, utekelezwaji wake ni jambo lingine.
“Kusaini mkataba ni jambo moja na Mkandarasi kufika eneo la mradi ni hatua nyingine, Daraja la Mto Malagarasi halitoshi bali tunaomba Barabara ya Nyakanazi nayo iwekwe lami,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Dodoma kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bi. Moza Abeid Said, alisema anaipongeza serikali ya CCM kwa kutekeleza ahadi zake, lakini zisifanywe karibu na uchaguzi kwani kilio cha barabara hizo ni cha muda mrefu.
Alisema ingawa yeye ni Mbunge kutoka upinzani, anaipongeza Serikali hasa inapotatua kero za wananchi bali wasiwasi mkubwa ni utekelezaji wake kwani wabunge wamekuwa wakilalamikia miradi mingi ambayo imesainiwa lakini haijatekelezwa.
“Waziri Magufuli ameweza kutekeleza ilani ya CCM katika sekta ya miundombinu ya barabara... amefanya kazi nzuri, barabara ya Babati-Iringa ikijengwa kama walivyosaini mikataba, itawasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Dodoma,” alisema.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ulitekelezwa kwa mkopo wa sh. bilioni 472 na awamu ya utatekelezwa kwa gharama ya sh. bilioni 538.88.
Alisema fedha zimetoka katika Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na nyingine kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambapo fedha nyingine zimetoka serikalini. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wabunge wote kutoka mikoa ya Manyara, Dodoma, Mtwara na Ruvuma ambao miradi hiyo inapita katika majimbo yao.







4 comments:

  1. NI VILE TU MAGUFULI RAIS KIKWETE ANAKUPIGA TAF ISINGEKUWA HIVYO VIKWAZO UNAVYOPATA UNGEJIUZULU

    ReplyDelete
  2. Hongera mzee Magufuli, Rais Mh.Kikwete akiwahutubia wananchi eneo la barabara ya kwa sadala Masama na baadaye ielekee Siha. Ulitoa siku 30, sasa yapata miaka miwili. Hakuna kilichofanyika. Wananchi wanaoishi kando ya barabara ya Bomangombe Kuelekea. Sanya juu walifanyiwa kiini macho mwaka na nusu sasa kwa maelezo wasindeleze maeneo yao hadi leo hatujui kinachoendelea. Baba njoo huku kutengua hiki kitendawili. Tujue la kufanya.

    ReplyDelete
  3. KWA KELI MAGUFULI UNAJITAHIDI SANA KEEP IT UP

    ReplyDelete